• May 5, 2024
  • Last Update May 4, 2024 8:34 PM
  • Nairobi

Wafanyibiashara wa pombe wasiofuata sheria waonywa

Wafanyibiashara wa pombe wasiofuata sheria waonywa

Molo,

Alhamisi Aprili 25, 2024

KNA na Emily Kadzo

Naibu kamishna wa gatuzi dogo la Rongai, William Kipchirchir ametoa onyo kali dhidi ya wale wanaoendeleza biashara ya mvinyo na pombe kali kinyume na sheria akisema kuwa watachukuliwa hatua kali ya kisheria.

Bwana Kipchirchir alisema kuwa wengi wa wale wanaomiliki maduka ya biashara za aina hiyo hufeli kuzingatia sheria kikamilifu baada ya kupokea leseni na hata kufichua kuwa wanaiendeleza biashara za uuzaji wa dawa za kulevya hata kwa vijana wa umri mdogo.

‘’Serikali kupitia ushirikiano na afisi ya leseni itaendelea kupiga doria na kuhakikisha kuwa hakuna biashara ya mvinyo na pombe kali inaendelezwa katika makazi na hata shule,’’ alinena Kipchirchir.

Aidha, alisema kuwa hataangalia vijana wengi wakipoteza maisha yao katika uraibu wa pombe na dawa za kulevya na hivyo basi kuwaomba washikadau wote hasa wazazi kushirikiana nao katika vita hivi ili kuona kuwa jamii inapata maadili mema yanayowezesha vijana kuendeleza maisha yao vyema.

‘’Unywaji wa pombe kupita kiasi huwakosesha vijana wengi maisha marefu na hata kuwanyima fursa ya kujenga taifa na hivyo basi tunapaswa kuwaelekeza mapema kabla ya mambo kwenda mrama ili waweze kujiendeleza vilivyo,’’ alisema Kipchirchir.

Aliongezea kuwa hata katika baa zile zinazomiliki leseni, hazitosazwa akisema kuwa zitachunguzwa kikamilifu mara kwa mara na iwapo watapatikana wamekiuka sheria basi watapokonywa leseni ya uendeshaji biashara hizo.

Kwa wale wanaouza pombe haramu nao walipewa onyo la kuhakikisha kuwa wanatii sheria na sio kuwafanyia mchezo wa paka na panya pale wanapopiga doria.

Hisani; KNA

Related Articles

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *