• May 17, 2024
  • Last Update May 17, 2024 12:30 PM
  • Nairobi

Wakaazi waombwa kuwa makini wakati wa mafuriko

Wakaazi waombwa kuwa makini wakati wa mafuriko

Molo,

Alhamisi, Mei 2, 2024

na Emily Kadzo/Millicent Asere

Serikali imejenga njia mbadala ya maji kutoka bwawa la Sagaitim lililoko eneo la Turi, katika gatuzi dogo la Molo ili kuepusha wakaazi na athari ya mafuriko iwapo maji yatavunja kingo zake.

Haya yalisemwa na kamishna msaidizi wa Molo, Job Williams katika ziara yake ya kukagua zaidi ya mabwawa matatu katika eneo hilo akisema kuwa bwawa la Sagaitim la kina cha futi 19 ndilo kubwa zaidi na hivyo basi ni muhimu kuchukua hatua ya tahadhari hata kama makaazi yako takriban mita 700 kutoka kwa bwawa.

Williams alizihakikishia zaidi ya familia tano zinazoishi umbali huu na bwawa la Sagaitim kuwa zipo katika maeneo salama lakini iwapo watapata wasiwasi kutokana na ongezeko la maji basi wasisite kuhamia katika maeneo yaliyo salama hadi pale viwango vya maji vitakaporudi sawa.

Katika mabwawa mengine aliyokagua ikiwemo Ngenda, Ndenderu B na Chandera, alisema kuwa hali iko shwari akiongezea kuwa mabwawa haya yako mbali na makaazi ya wakaazi wa maeneo hayo.

Aidha aliwatahadharisha wakaazi kutokuwa na uzoefu wa kwenda kufanyia shughuli zao karibu na mabwawa kutokana na mvua kubwa inayoendelea kunya ili kuzuia maafa ya aina yoyote ile.

Tayari, serikali ya kaunti ya Nakuru kupitia wizara ya maji imeweka timu ambayo imetambua mabwawa yote na yale ambayo yako katika hatari ya kufurika, yanapunguziwa maji kupitia njia mbadala ili kuzuia athari kubwa za mafuriko.

Wiki jana, kaunti ya Nakuru ilikumbwa na mkasa wa mafuriko katika eneo la Mai Mahiu baada ya mto kutoka upande wa Kijabe kuvunja kingo zake na kusababisha vifo vya watu zaidi ya 50 na uharibifu mkubwa wa mali.

Hisani; KNA

Related Articles

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *